Watanzania watoa mkono wa pole msiba wa wanafunzi Shule ya Lucky Vincent - Arusha


Watanzania watoa mkono wa  pole  msiba wa wanafunzi Shule ya Lucky Vincent - Arusha

Leo tarehe 19.5.2017 taasisi za TiME Tickets, Eco Valley Advisers, na Clouds Media wamekabidhi kwa uongozi wa mkoa wa Arusha waliopokea kwa niaba ya wafiwa, kiasi cha shilingi 4,444,031/- ikiwa ni rambi rambi zilizochangwa na watanzania kupitia mfumo wa harambee wa WEZESHAsasa (www.wezeshasasa.com). Fedha hizo zimepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Mrisho Gambo.

“Kama ilivo desturi ya Watanzania kuitikia kwa vitendo kusaidia  kwa hali na mali pindi mtu, kikundi au jamii inapopatwa na majanga yasiyotarajiwa, taasisi za Clouds Media, Eco Valley Advisers na TiME Tickets walikubaliana kwa pamoja na kwa dhati kuunganisha nguvu za Watanzania wote pasipo kujali dini, hali, itikadi, jinsi na maeneo ya  kijiografia wakiwa na dhamira ya kuhamasisha rambi rambi kwa takribani siku 4 ( 8 – 11 Mei 2017)”  Alisema  mkurugenzi wa TiME Tickets, Bwana Josephat Mandara.

Ndani ya kipindi hicho kifupi kisichozidi siku nne, wachangiaji wapatao 721 (huku watu 10 wakichanga zaidi ya mara moja, kufanya michango 731) waliweza kuchangia kiasi cha pesa za Kitanzania zipatazo shilingi 4,444,031/-. Wachangiaji wote na kiasi cha machango cha kila mmoja yanaweza kupatikana hapa. Jambo la kuzingatia na ambalo ni faraja kwa wote walioratibu zoezi hili sio wingi wa pesa wala idadi ya wachangiaji bali ni uwezo wa mfumo kuweza kuwaleta pamoja Watanzania wote. Sura pana ya utaifa inajidhihirisha kwenye aina ya michango. Kwa mujibu wa mtiririko wa uchangiaji, michango iliyopatikana ni kati ya shilingi 10/- hadi shilingi 700,000/- Tafsiri  ya aina hii ya uchangiaji ni kwamba mfumo umeweza kuimarisha mshikamano wa Watanzania. Idadi hii ya watu na kiwango cha pesa vimepatikana kwa uwazi kama inavyoonekana katika tovuti. www.wezeshasasa.com/lucky

Kwa kuzingatia malengo ya ukusanyaji wa rambi rambi kama yalivokuwa yameainishwa kwenye tovuti, kila familia ya wafiwa  itapokea kiasi cha shilingi 126,972/-  Katika makabidhiano hayo mkuu wa mkoa  wa Arusha  Mh. Mrisho Gambo alisema “ Kwa niaba ya wafiwa na wananchi wa Arusha tumefarijika sana kuona kwamba Watanzania kwa umoja wao  wamekuwa nasi katika kipindi hiki cha majonzi. Ni jambo la kutia moyo na kujivunia kwamba sasa upo mfumo wa harambee wa TEHAMA na ubunifu ambao unaweza kukusanya michango kwa ufanisi na uwazi”.

Makabidhiano ya rambi rambi yalifanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kushudiwa na Katibu Tawala wa mkoa Bw. Richard N. Kavitega, uongozi wa Shule ya Lucky Vincent na waadishi wa habari.

Unaweza kupata nakala ya taarifa ya makabidhiano (press release) hapa.
Kuona wachangiaji wote na kiasi chao walichotoa pakua dokumenti hii.

 

Watanzania watoa mkono wa  pole  msiba wa wanafunzi Shule ya Lucky Vincent - Arusha